PROSHABO ONLINE SCHOOLS Swahili,WISDOM GUIDANCE TUKIPENDE KISWAHILI MAANA SASA NI LUGHA YA KIMATAIFA

TUKIPENDE KISWAHILI MAANA SASA NI LUGHA YA KIMATAIFA



Categories:

Siku chache kabla ya kuanza kwa mkutano mkuu wa mazingira, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) limezindua tovuti mpya itakayotumia Kiswahili ili kuwafikia mamilioni ya wazungumzaji wa lugha hiyo duniani. 

Mkutano huo utakaendeshwa jijini New York, Marekani utafanyika Septemba 23. Akizindua matumizi ya Kiswahili, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Dkt. Joyce Msuya (pichani) amesema shirika hilo litatoa nafasi kwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili kushirikiana UNEP kuzikabili changamoto za mazingira. “Kiswahili ni lugha inayotujumuisha Afrika Mashariki, kusini mwa Afrika na pembe zote duniani. Leo tunafuraha mno kuanzisha mtandao na tovuti ya Kiswahili ya Shirika la Mazingira. Hii ni nafasi nzuri sana kwenu nyie kushirikiana nasi katika changamoto za mazingira na kwetu sisi kusikia maoni yenu kuhusu kazi zetu,” anasema Dkt. Msuya.

    Licha ya tovuti, shirika hilo pia litatumia lugha ya Kiswahili kwenye mitandao yake ya kijamii kujadili changamoto za hali ya hewa, bayoanuai, uchafuzi wa hewa na kupokea mapendekezo ya masuluhisho ya changamoto zilizopo za mazingira pamoja na masuala mengine.

“Katika azma ya kuwafikia mamilioni ya wazungumzaji wa Kiswahili kote duniani, tovuti hii na mitandao ya kijamii, itasambaza habari kuhusu mazingira, itatoa takwimu muhimu, na inanuia kuchapisha matukio ya watu wanaofanya juhudi ili kuboresha mazingira yetu,” anasema Dkt. Msuya.

Hatua hii ya UNEP imechukuliwa siku chache baada ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuridhia Kiswahili kuwa lugha rasmi itakayotumika kwenye mikutano na shughuli zake nyingine.

 Uamuzi huo ulichukuliwa kwenye mkutano mkuu wa 39 wa SADC  uliofanyika mwezi uliopita jijini Dar es Salaam na kuifanya jumuiya hiyo kutumia Kiingereza, Kifaransa, Kireno na Kiswahili kwenye mawasiliano ya kikazi.

 Wakati SADC  ikikipeleka Kiswahili miongoni mwa nchi 16 wanachama wake, UNEP iliyoanzishwa Juni 5, 1972 inakipa hatua ya ziada kwa kukifikishwa kwa wananchi wote wanaofuatilia habari zake duniani.    Mwalimu wa Kiswahili katika Chuo cha Kumbukumbu ya Julius Nyerere kilichopo Kigamboni, Joseph Isindikiro anasema kujipenyeza kwa lugha hii katika nchi na mashirika ya kimataifa kunatoa matumaini kwa wanazuoni wake.

“Uzinduzi wa tovuti hiyo unamaanisha Kiswahili ipo kwenye hatua nzuri kuwa lugha rasmi ya Umoja wa Mataifa. Shirika la Mazingira limegundua kuna watu wengi wanaokosa taarifa zake kutokana na kutozielewa lugha inazotumia,” anasema Isindikiro.

Umoja wa Mataifa na mashirika yake kwa sasa unatumia lugha sita kwenye mawasiliano yake ambazo ni Kiarabu, Kifaransa, Kichina, Kiingereza, Kihispaniola na Kirusi.

Kiswahili kuzungumzwa katika  nchi za Tanzania, Burundi, DRC, Kenya, Rwanda, Somalia na Uganda. Pia, Mayotte, Msumbiji, Afrika Kusini, Falme za Kiarabu, Oman na Marekani.

Leave a Reply